Uchafuzi wa hewa unaweza kutokea katika eneo letu, lakini unaweza kusafiri mbali mno, wakati mwingine katika mabara kwenye ruwaza za hali ya hewa ya kimataifa.
Uchafuzi wa hewa hutokana na vitu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kaboni monoksidi, kaboni dioksidi, nitrojeni dioksidi, nitrojeni oksidi, ozoni ya kiwango cha chini, chembe chembe, salfa dioksidi, haidrokaboni na risasi - vyote vikiwa hatari kwa afya ya binadamu.
NYUMBANI
Chanzo kikuu cha uchafuzi wa hewa wa nyumbani ni kuchoma fueli ya visukuku, kuni na fueli ingine inayotokana na mimea ndani ya nyumba kupikia, kupasha nyumba joto na kutoa mwangaza. Karibu vifo vya mapema milioni 3.8 husababishwa na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba kila mwaka, idadi kubwa kati ya vifo hivyo ni katika nchi zinazoendelea.
Nchi 97 kati ya nchi 193, zimeongeza asilimia ya familia ambazo zinapata fueli isiyochafua mazingira inapochomwa kwa zaidi ya asilimia 85. Hata hivyo, watu bilioni 3 wanaendelea kutumia fueli mango na moto wazi kupika, kupasha joto na kutoa mwangaza. Matumizi ya majiko ya kisasa zaidi na fueli zisizochafua mazingira kunaweza kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa na kuokoa maisha.
VIWANDA
Katika nchi nyingi, uzalishaji wa nishati ni chanzo kinachoongoza cha uchafuzi wa hewa. Mitambo ya kuchoma makaa ya mawe inachangia pakubwa, wakati jenereta za dizeli ni tishio kwa maeneo yasiyofikiwa na umeme. Michakato ya viwanda na matumizi ya viyeyushi, katika viwanda vya kemikali na madini, pia huchafua hewa.
Sera na programu zinazolenga kuimarisha ufanisi wa nishati na uzalishaji kutoka kwa vyanzo vinavyoweza kutumika tena ina athari ya moja kwa moja kwa ubora wa hewa ya nchi. Kwa sasa, nchi 82 kati ya 193 zina ruzuku ambazo zinakuza uwekezaji katika uzalishaji wa nishati inayoweza kutumika tena, uzalishaji usiochafua mazingira, matumizi ya nishati kikamilifu na au udhibiti wa uchafuzi wa mazingira.
UCHUKUZI
Sekta ya uchukuzi ulimwenguni inawajibikia karibu robo moja ya uchafuzi unaohusiana na kaboni dioksidi, kiwango ambacho kinazidi kuongezeka. Uchafuzi huu unaotokana na uchukuzi umehusishwa na takribani vifo 400,000 vya mapema. huku karibu nusu ya vifo hivi vikitokana na uchafuzi wa dizeli. Wale wanaoishi karibu na sehemu kubwa ya trafiki wana uwezekano wa hadi asilimia 12 kugunduliwa kuwa na matatizo ya kiakili.
Kupunguza uchafuzi kutoka kwa magari ni hatua muhimu ya kuboresha hali ya hewa, haswa katika maeneo ya mijini. Sera na viwango vinavyohitaji matumizi ya fueli zisizochafua mazingira na viwango vya juu vya magari yasiouchafua zinaweza kupunguza uchafuzi wa magari kwa asilimia 90 au zaidi.
KILIMO
Kuna vyanzo viwili vikuu vya uchafuzi wa hewa kutoka kwa kilimo: mifugo, ambayo hutoa methani na amonia, na kuchoma taka za kilimo. Uchafuzi wa methani unachangia ozoni ya kiwango cha chini, ambayo husababisha pumu na magonjwa mengine ya mfumo wa kupumulia. Baada ya kupimwa kwa kipindi cha miaka 20, methani ina uwezo zaidi ya mara 80 kuliko kaboni dioksidi wa kuongeza joto duniani. Karibu asilimia 24 ya gesi zote za ukaa zinazotolewa angani ulimwenguni zinatokana na kilimo, misitu na matumizi mengine ya ardhi.
Kuna njia nyingi za kupunguza uchafuzi wa hewa kutoka kwa kilimo. Watu wanaweza kuhamia kwenye lishe inayotegemea mimea na kupunguza taka ya chakula, wakati wakulima wanaweza kupunguza methani kutoka kwa mifugo kwa kuimarisha lishe na kuboresha usimamizi wa sehemu za malisho na nyanda.
TAKA
Uchomaji wazi wa takataka na taka zinazoweza kuoza kuoza katika maeneo yaliyo wazi pia huachilia dioksini hatari, furani, methani na kaboni nyeusi angani. Ulimwenguni kote, inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya taka huteketezwa hadharani. Tatizo hili ni kubwa zaidi katika maeneo ya miji na nchi zinazoendelea. Uchomaji wazi wa taka za kilimo au za manispaa hufanywa katika nchi 166 kati ya 193.
Kuboresha ukusanyaji, kutenganisha na utupaji wa taka hupunguza kiwango cha taka mango ambazo zinachomwa au kujazwa ardhini. Kutenganisha taka inayoweza kuoza na kuibadilisha kuwa mbolea au nishati kutoka kwa mimea inaboresha rutuba ya mchanga na hutoa chanzo mbadala cha nishati. Kupunguza makadirio ya theluthi moja ya chakula chote ambacho kinatupwa au kuharibika pia kunaweza kuboresha hali ya hewa.
VYANZO VINGINE
Sio uchafuzi wote wa hewa unatokana na shughuli za binadamu. Mlipuko wa volkano, dhoruba za vumbi na michakato mingine ya asili pia ni changamoto. Dhoruba za mchanga na vumbi zinatia wasiwasi sana. Chembe ndogo za vumbi zinaweza kusafiri maelfu ya maili kwenye dhoruba hizi, ambazo zinaweza pia kubeba vimelea vya magonjwa na vitu vyenye madhara, na kusababisha matatizo makali na ya kudumu ya kupumua.
Hapa kuna njia chache tunazoweza kutumia kukabiliana na vyanzo vya uchafuzi wa hewa:
- Tumia sauti yako na pesa zako kupiga kura. Unaweza kutoa wito kwa serikali na kwa mashirika ya biashara kuchukua hatua madhubuti. Kama mtu binafsi unaweza kubadilisha unavyoishi kupunguza matumizi ya mafuta na nishati, kutupa chakula kidogo na kadhalika.
- Serikali zinaweza kupitisha na kutekeleza viwango vya mazingira vya kiwango cha kimataifa kwa fueli isiyochafua mazingira, na kutoa magari yasiyochafua mazingira na yanayotumia nishati vizuri.
- Miji inaweza kuunda mifumo madhubuti ya usafiri wa umma na mipango ya usafirishaji ambayo inatoa kipaumbele kwa kutembea, matumizi ya baiskeli, na usafiri wa umma.
- Wafanyabiashara wanaweza kuchukua hatua moja kwa moja kwa kupunguza uchafuzi wao na kuanzisha teknolojia mpya kutusaidia kuishi bila kuchafua mazingira, bila taka nyingi.
Ikiwa sote tutachukua hatua, tunaweza kupumua kwa urahisi zaidi. Hatuwezi kufaulu bila wewe.